Lowassa, Membe na Kikwete CCM kichwa kinauma!
pichani: raisi Kikwete na waziri mkuu mstaafu EDWARD LOWASA |
Dar es Salaam. Vigogo sita wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambao walipewa onyo
kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 wamezidi kukitesa chama hicho,
na katika kuwadhibiti, kimetoa maagizo kwa Kamati ya Usalama na Maadili
kufuatilia nyendo zao.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika
kikao cha kawaida cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu jijini Dar es
Salaam, kuwa kamati hiyo ifanye mapitio ya mwenendo wa utekelezaji wa adhabu
kwa vigogo hao waliotiwa hatiani kwa kufanya kampeni za urais kabla ya wakati.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Vigogo hao ambao wamekuwa wakitajwa
na wakati mwingine wenyewe kuzungumzia nia ya kushika nafasi hiyo, walipewa
onyo kali ikiwamo kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 tangu Februari mwaka
huu ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokiuka maadili ya
chama hicho.
Vigogo hao walipatikana na makosa ya
kuvunja ibara ya 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inayozuia
kutoa michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya
kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo
husika.
Jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema mwezi ujao kamati hiyo itafanya
mapitio ya utekelezaji wa adhabu hiyo ili kubaini iwapo wanaitekeleza au la.
“Kama itabainika kuwa hawatekelezi
ipasavyo masharti ya adhabu zao, itapendekezwa kwa Kamati Kuu ili waongezewe
adhabu nyingine kufuatana na taratibu za chama,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa Nnauye, Kamati Kuu
imepokea taarifa za kuwapo kwa harakati za baadhi ya wanachama walioonyesha nia
ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina Kamati
Kuu inawakumbusha kuwa ili wanachama hao wasipoteze sifa za kugombea, ni muhimu
wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia masuala hayo,”
alisema Nnauye.
Tangu wapewe adhabu hiyo, makada hao
wamekuwa wakijitokeza hadharani kwa nadra, lakini Makamba na Wassira
walikaririwa na vyombo vya habari wakitangaza nia ya kugombea urais.
Hata hivyo, CCM ilisema kuwa Makamba
hakukiuka taratibu kwa kutangaza nia hiyo, ingawa Rais Jakaya Kikwete alisema
mtoto huyo wa katibu mkuu wa zamani wa chama hicho anataka mambo makubwa na
hakumtaarifu nia hiyo.
Comments
Post a Comment