Afisa Balozi afukuzwa kazi Zanzibar.TAHARIFA KWA HUMA.
Na Jabir Idrissa, Zanzibar
HATIMAYE Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman, amefutwa kazi. Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein ametangaza kumfuta kazi Othman; na nafasi yake tayari imechukuliwa na naibu wake, Said Hassan Said, imeeleza taarifa ya serikali.
Taarifa hiyo iliyosomwa kwa vyombo vya habari juzi inasema, Othman amefutwa kazi kwa mujibu wa vifungu vya 53, 54(1) na 55(3) vya Katiba ya Zanzibar ya 1984 na kifungu 12 (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 2 ya 2011.
Taarifa za kufutwa kazi kwa Othman zilisambaa jioni ya juzi kupitia vituo vya televisheni, ambavyo vilieleza kuwa Dk. Shein alimfuta kazi mwanasheria huyo. Hakutaja sababu isipokuwa vifungu vya sheria.
Othman alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba waliopiga kura ya HAPANA kwa katiba inayopendekezwa.
Mwanataaluma huyo ambaye awali aliondoka bungeni, alirejea siku ya mwisho ya upigaji kura; ambapo alikataa karibu theluthi mbili za ibara zote za katiba iliyopendekezwa. Katiba hiyo ina Sura 71 na Ibara 289.
Wakati Othman akifutwa kazi, ofisa mwingine wa ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, anadaiwa kuagizwa kurejea nchini.
Ofisa aliyeagizwa kurejea nchini amefahamika kwa jina moja la Masoud. Ni mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa anayetokea Zanzibar.
Mfanyakazi huyo ambaye ni afisa wa ngazi ya juu, ndiye aliandika barua akionesha kuwa mazingira yaliyoko maeneo ya Makkah, Saudia, hayangeruhusu wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kupiga kura.
MAWIO limefahamishwa kuwa barua hiyo iliyosainiwa kwa niaba ya Balozi, ikiwa ni majibu ya barua ya awali iliyotoka Ofisi ya Bunge Maalum, mjini Dodoma, ilieleza kwa ufasaha katika aya ya mwisho, kwamba “haitawezekana wajumbe wa Bunge Maalum kupiga kura.”
Taarifa kutoka Saudi Arabia na mjini Dodoma zinasema, barua hiyo tayari imeleta mgogoro ndani ya serikali, baada ya kufichuka kwa siri juu ya kinachoitwa “theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar.”
Masoud, kwa wadhifa wake ubalozini, ni miongoni mwa maofisa walioidhinishwa kusaini barua kwa niaba ya balozi.
“Ni kweli wametaka arejee nchini haraka. Hivi ninavyokwambia Masoud tayari ameondoka Riyadh kurejea huko (Tanzania). Lakini hapa ubalozini, msimamo uko wazi, kwamba hakuna kosa alilolitenda,” anaeleza mtoa taarifa ndani ya ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.
Amesema, “Sasa Masoud ni mmoja wa maofisa wachache walioidhinishwa kulingana na nyadhifa walizonazo, kusaini barua yoyote kwa niaba ya balozi, kwa hivo hajatenda kosa lolote la kinidhamu.”
Taarifa zinasema, balozi amekuwa zaidi katika maeneo ya Makkah kusimamia usalama wa mahujaji wa Tanzania wakiwemo wake wa viongozi kadhaa wa kitaifa; jambo ambalo lilimlazimisha Masoud kufanya kazi hiyo kwa niaba yake.
Barua iliyosainiwa na Masoud, tayari imevuja katika mitandao ya kijamii.
“Unajua Balozi amekuwa hayupo hapa Riyadh muda mwingi. Yeye anashughulikia masuala ya usalama wa mahujaji Makkah; kwa hivyo tuliopo Riyadh ndio tunatekeleza kazi tunazotakiwa kuzifanya,” alisema mtumishi mwingine.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya Bunge Maalum zinasema mazingira yaliyokuwepo Makkah, wakati wa ibada ya Hijja, hayakuwezesha wajumbe wa bunge hilo walioko katika ibada hiyo, kupiga kura kama ilivyotarajiwa.
Katika hatua nyingine, watu mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wanasema kilichotokea Dodoma katika kupiga na kuhesabu kura, kitakuwa “kitendawili kikubwa.”
“Kila nikipima nakuta ninaumizwa na utamaduni wa kikulacho kinguoni mwako. Kwamba wapo wenzetu hawajali maslahi ya nchi isipokuwa matumbo yao,” ameeleza Omar Said wa Michenzani.
Naye Rashid Sultani anayeishi Mkunazini, Unguja amesema, itamchukua muda mrefu kuamini kuwa theluthi mbili ya kura za wajumbe wa Zanzibar ilifikiwa.
Suala la kufutwa kazi Othman, kuitwa nyumbani kwa ofisa wa ubalozi na mjadala juu ya theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar, ni miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Chama cha Wananchi (CUF), Jumapili hii mjini Zanzibar.
Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya CUF imesema Katibu Mkuu wa Chama na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, ndiye atakakuwa msemaji mkuu.
Chanzo: Mawio
Mambobomba inasisitiza uwajibikaji na uhaminifu kwa wafanyakazi wote wenye dhamana.
Comments
Post a Comment