CHADEMA YAANDAMANA JIJINI DAR-ES-LAAM KUMSHINIKIZA RAIS KIKWETE AVUNJE BUNGE LA KATIBA
CHAMA
 cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Dar es Salaam, jana 
kimetoa tamko la kufanya maandamano ili kumshinikiza Rais Jakaya 
Kikwete, alivunje Bunge Maalumu la Katiba.
Pia
 chama hicho kinatarajia kutoa tamko juu ya kauli aliyoitoa Mwanasheria 
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema juu ya Umoja wa Katiba ya 
Wananchi (UKAWA).
Tamko
 hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi Mkoa Bw. John Mnyika
 ambaye ni mbunge wa Ubungo, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika 
Viwanja vya Hananasifu.
Awali
 akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA mkoani humo,
 Enry Kilewo, alisema tamko hilo ni azimio ambalo lilifikiwa kwenye 
kikao cha baraza hilo mkoa.
Alisema uongozi wa chama hicho mkoa, umetangaza rasmi kuanza mchakato wa kuwania nafasi za uongozi mkoa.
Alisema
 awali Baraza la Wazee lilikaa hivi karibuni na kupokea taarifa za mikoa
 ya uchaguzi ambayo ni Kinondoni, Ilala na Temeke ambapo katika Mkoa wa 
Kinondoni, wilaya za uchaguzi za Ubungo na Kawe zilionekana kuwa na 
matatizo kwenye nafasi ya Mwenyekiti baada ya wagombea wote kutofikia 
kura asilimia 51.
Aliongeza
 kuwa, baada ya kupokea taarifa hizo uchaguzi huo sasa utarudiwa Agosti 
23, mwaka huu ambapo katika Wilaya ya Kawe, Powery Mfinanga alichaguliwa
 kuwa Mwenyekiti baada ya kupata kura asilimia 62 na kumshinda mpinzani 
wake Remy Mbidu aliyetepata asilimia 37.6.
“Kutokana
 na chaguzi ndani ya Mkoa kukamilika kwa asilimia 99, Katiba inaturuhusu
 kuitisha uchaguzi wa Mkoa…fomu za kugombea nafasi mbalimbali zimeanza 
kutolewa Agosti 17, mwaka huu, mwisho wa kurudisha ni Agosti 20, mwaka 
huu, saa 10:30 jioni na uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Agosti 24, mwaka 
huu,” alisema.
Alisema
 fomu za uchaguzi zinapatikana katika ofisi zote za chama katika mkoa 
huo lakini wakati wa kurudishwa, zinatakiwa kurudishwa kwenye ofisi ya 
mkoa iliyoko Mwananyamala na baada ya hapo zitapelekwa ngazi ya Taifa 
ili kufanyiwa usaili kwa kushirikiana na uongozi wa kanda.
Nafasi
 zinazogombewa ni Mwenyekiti Mkoa ambayo hivi sasa inashikiliwa na Bw. 
Mnyika, Katibu Mkuu Mkoa (Kilewo), Mwenyekiti Baraza la Wanawake Mkoa 
(BAWACHA) inayoshikiliwa na Suzan Lyimo na Katibu wake (Joyce Msuya), 
ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu.
Nafasi
 nyingine ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa (Hawa Mwaifunga), Katibu
 wake (Renatus Mlashani), Mwenyekiti Baraza la Wazee Mkoa (Erasto 
Sibila), Katibu wake nafasi iko wazi.
Hivi
 karibuni viongozi wa vyama vinavyounda UKAWA, walimtaka Rais Kikwete 
alisitishe Bunge la Katiba na kudai kama halitasitishwa wataitisha 
maandamano makubwa nchi nzima.

 
 
 
Comments
Post a Comment