RAIS KIKWETE ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA JAJI LEWIS MAKAME


Marehemu Jaji Mstaafu, Lewis Makame enzi za uhai wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, National Electoral Commission (NEC) kufuatia taarifa za kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu, Mheshimiwa Lewis Makame kilichotokea katika Hospitali ya AMI Trauma Centre Jijini Dar es Salaam tarehe 18 Agosti, 2014.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania na Mwenyekiti wa Kwanza wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) chini ya Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, Mheshimiwa Lewis Makame ambaye amelitumikia Taifa letu katika Utumishi wa Umma kwa uaminifu, uadilifu, bidii na umahiri mkubwa”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake.
Katika utumishi wake, Marehemu Jaji Lewis Makame, enzi za uhai wake, alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kabla ya kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa na baadaye Mwenyekiti wa NEC ambayo aliiongoza kwa miaka 17 mfululizo hadi alipostaafu mwaka 2011. Uongozi wake ulichangia sana kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa katika mazingira mapya ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa hapa nchini.
“Ni kwa kutambua kipaji kikubwa cha uongozi alichokuwa nacho Marehemu Jaji Lewis Makame, Taifa letu limepoteza mtu muhimu sana kwani hata baada ya kustaafu kwake alikuwa bado anahitajika sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika mambo mengi yanayohusu maendeleo ya nchi yetu”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,
“Kutokana na msiba huu mkubwa, nakutumia Salamu za Rambirambi kwa kumpoteza aliyekuwa Kiongozi Mahiri wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kupitia kwako, naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi ziifikie Familia ya Marehemu kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu, Jaji Lewis Makame, Amina”, amesema Rais Kikwete akiomboleza msiba huu.
Amewahakikishia Wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema awape moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira Wanafamilia wote, ndugu na jamaa wa Marehemu, ili waweze kuhimili machungu ya kuondokewa na Mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni Mapenzi yake Mola.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Agosti, 2014

Comments

Popular posts from this blog

STYLE KALI:TUMIA HII NDANI YA DAKIKA MOJA TU MWANAMKE AMEKOJOA.

KISIMI (kinembe) kikichezewa mwanamke anaweza kuwataja maawara zake wote.