MASAA 72 BAADA YA PINDA KUTANGAZA NIA YA KUWANIA URAISI W JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MAKADA WA CCM ROHO JUU.
Mzee wa busara Mh.MIZENGO PETER PINDA .baada ya kutangaza nia ya kugombea uraisi mwaka 2015.
SIKU
moja baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutangaza nia ya kujitosa
kuwani urais katika Uchaguzi Mkuu 2015, baadhi ya wanachama wa CCM na
wasomi wamekuwa na maoni tofauti.
Hali
hiyo imekuwa tofauti ambapo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip
Mangula, alishindwa kueleza kwa undani kauli hiyo ya Pinda huku akisema
hawezi kuzungumza jambo lolote kwa sasa hadi pale atakapomaliza vikao
vya chama.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu, Mangula alisema: “Kwa sasa sina la kusema kuhusu suala hili kwani nipo kwenye vikao, ninaomba nitafute baadaye ndugu yangu,” alisema kwa kifupi.
Mangula
ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Nidhamu na Maadili ya CCM, hivi
karibuni alitangaza mikakati ya chama katika kuwadhibiti wagombea
wanaotangaza nia za kuwania nafasi za uongozi ikiwemo urais kabla ya
wakati kwa kuwafungulia majalada kila mkoa kwa ajili ya kufuatilia
mienendo ya wagombea hao.
Pamoja na kuomba atafutwe baada ya saa mbili, MTANZANIA lilifanya hivyo na simu yake alikuwa amezima hadi tunakwenda mitamboni.
Pamoja
na hali hiyo, MTANZANIA pia lilimtafuta Katibu wa NEC, Itikadi na
Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ambaye simu yake
iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu
hakujibu.
Akizungumzia
uamuzi huo wa Pinda, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy Mohamed
(CCM), alimmwagia sifa Waziri Mkuu Pinda kwa kusema ni kiongozi mwenye
uwezo na asiye na kashfa ya aina yoyote ndani na nje ya Serikali.
Alisema
kuwa kutokana na sifa yake hiyo, ni wazi kiongozi huyo wa Serikali
hakukurupuka kuitaka nafasi hiyo ya uongozi wa juu ya nchi.
Hata
hivyo, alipoulizwa kuhusu mkakati wake wa kugawa fedha kwa wajumbe wa
CCM waliokwenda katika kikao chake, Keissy alisema hakubaliani na
taarifa hizo kwa Waziri Pinda kutoa kiasi cha Sh 50,000 kwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu wa CCM Taifa waliofikia 50 toka katika mikoa sita ya Kanda
ya Ziwa.
Wajumbe
wa mikoa hiyo wanaodaiwa kupewa kila mmoja Sh 50,000 kwa ajili ya fedha
za nauli ni wa kutoka kwenye mikoa ya Simiyu, Mwanza, Geita, Mara,
Shinyanga na Kagera ambao walikutana na Waziri Mkuu Pinda Ikulu ndogo ya
jijini Mwanza.
“Hiyo
si kweli kwani Waziri Pinda namjua hana fedha hiyo ya kuwagawia wajumbe
wote hao, lakini kama kweli katoa atakuwa amefanya makosa, ila kwa
kutangaza nia bado si kosa kwani kosa ni kufanya kampeni,” alisema.
Kwa
upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es Salaam Kitivo
cha Elimu (DUCE), Profesa Kitila Mkumbo, alisema kwa sasa hawezi
kuzungumzia jambo liolote kuhusu kufaa au kutofaa kwa Waziri Pinda
kuwania urais mwaka 2015.
“Imekuwa
kawaida kwa mawaziri wakuu wa nchi hii kila mmoja pindi anapomaliza
muda wake kutangaza nia ya kuwania urais, hivyo kwa suala la Pinda kama
anafaa au hafai sina ‘comment’ kwa hilo,” alisema Profesa Kitila.
Inadaiwa
Pinda pamoja na kugawa fedha hizo kwa kumtumia mmoja wa watu wake wa
karibu, kugawa nauli ya Sh 50,000 kwa kila mjumbe, ambapo wajumbe hao
waligomea posho hiyo kwa kueleza kuwa ni ndogo.
Pia
Waziri Mkuu Pinda anatuhumiwa kutumia harambee ya Taasisi ya Benjamin
Mkapa kujiimarisha kisiasa, kwani tayari CCM imepiga marufuku kwa
viongozi wake na makada wake kuendesha harambee zozote zile zenye
malengo ya kujiimarisha.
Waziri
Mkuu Pinda aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya kujitathimini na
kupokea ushauri toka kwa baadhi ya maaskofu hapa nchini, kwa nia ya
dhati kabisa ameamua kugombea urais kupitia CCM na kuwataka wajumbe hao
wa mkutano mkuu kumuunga mkono.
Waziri
Mkuu Pinda anadaiwa kuwaeleza wajumbe hao kuwa awali hakuwa na nia ya
kugombea nafasi hiyo kutokana na mazingira ya nafasi yenyewe yalivyo, na
kueleza kuwa hivi sasa ana ujasiri wa kugombea nafasi hiyo.
Waziri
Mkuu Pinda anadaiwa kueleza wajumbe hao kuwa ana siri nzito moyoni kwa
kuwa yeye ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili, Kamati Kuu (CCM) na NEC na
kutamba kuwa ana uhakika jina lake ni miongoni mwa majina matano ambayo
yatapendekezwa na CC.
Alisema
kuwa kutokana na mazingira hayo, ndio maana ameamua kukutana na wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kwa ajili ya kuwaeleza nia yake ya
kugombea nafasi hiyo ili waweze kumuunga mkono.
Kauli tata za Pinda
Januari
25, mwaka 2012, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitamka hadharani kwamba
hana nia wala hataki kuwania urais mwaka 2015 Rais Jakaya Kikwete
atakapomaliza muda wake, kwa kuwa kazi hiyo ni mzigo.
Badala
yake alisisitiza kuwa hatajisumbua kuingia katika kinyang’anyiro hicho
kwani amejipanga vyema kuanza maisha mapya ya kufuga nyuki baada ya
kustaafu.
Kauli
hiyo ya Pinda aliitoa mbele ya wahariri na waandishi wa habari kuhusu
mwelekeo wa nchi na masuala muhimu ya kitaifa yaliyojitokeza siku za
hivi karibuni.
Alisema mwaka 2015 atakuwa mtu mzima sana na haamini kuwa kwa umri huo ataweza kuyamudu majukumu ya nafasi ya urais.
“Niliposema
sitawania urais nilimaanisha hivyo na naomba watu wanielewe, urais si
kazi ya kukimbilia kama kweli unataka kuwatumikia watu, kwa wale
wanaotaka kwenda kuchuma sawa ni pazuri, lakini mimi naona ni mzigo,
kuna wakati namwonea huruma Rais Kikwete maana kila kitu kigumu
anaangushiwa yeye,” alisema.
“Mwaka
2015 nitakuwa na umri wa miaka 67, ina maana nikipata urais baada ya
miaka mitano nitakuwa na 72, yanini nifike kote huko kwanini wakati
nimeshalitumikia taifa langu muda mrefu sana, nimefanyakazi ya taaluma
yangu ya sheria miaka mitatu tu nikaenda Ikulu ambako nimefanyakazi hadi
leo hii, nimefanyakazi na Mwalimu Nyerere, nimefanyakazi na Mzee
Mwinyi, Mzee Mkapa na hii awamu ya nne, kama watu hawajaridhika na
mchango nilioutoa kwa nchi yangu inamaana hata nikiwa nani
hawataridhika. Urais siutaki na wala siwazii wanaotaka waendelee tu,” alisema.
“Kuna
wakati nikisema sitaki urais watu wananiambia acha kusema hivyo wewe,
acha kabisa mzee usiseme hivyo, lakini mimi huwa nawaambia watu hawa
kuwa huu ni uamuzi wangu na nataka Watanzania waelewe hivyo, anayetaka
haya! Ila mimi sitakuwemo,” alisema.
Alisema
anataka baada ya kustaafu ajikite zaidi katika ufugaji wa nyuki kwani
amebaini kuwa biashara hiyo ina faida sana lakini Watanzania wengi bado
hawajabaini fursa hiyo.
chanzo: Mtanzania
chanzo: Mtanzania
Comments
Post a Comment